Luka. 2: 22-40 | Kutakasika kwa Yesu | Familia takatifu | Yesu Maria Yosefu | Mshairi Pendo
ฝัง
- เผยแพร่เมื่อ 6 ม.ค. 2025
- Jumapili ya 29/12/2024
Luka. 2: 22-40
Kutakasika kwa Yesu
(K)Wokovu lotuwekea, kwa macho tumeuona.
1.Siku zilipotimia, za Yesu kutakasika.
Torati livyotakia, Musa alivyoandika.
Yosefu liitikia, mwanao kutakasika.
Wokovu lotuwekea, kwa macho tumeuona.
2.Walifika hekaluni, na sadaka mikononi.
Hua wawili kapuni, kwa upendo na shukrani.
Kutimiza ya zamani, ilivyosemwa zamani.
Wokovu lotuwekea, kwa macho tumeuona.
3.Na pale Yerusalemu, kulikuwa Simeoni.
Mwenye haki na fahamu, yake Mungu hekaluni.
Israeli pate hamu, ya wokovu utumwani.
Wokovu lotuwekea, kwa macho tumeuona.
4.Na Roho alimwonyani, mauti hatayaona.
Hadi mwokozi ajeni, hekaluni kukutana.
Limbeba mikononi, na kufurahia mwana.
Wokovu lotuwekea, kwa macho tumeuona.
5.Akasema kwa shukrani, moyo mejawa amani.
"Mtumishio Manani, mwachilie kwa amani.
Nimeuona machoni, wokovu wa duniani".
Wokovu lotuwekea, kwa macho tumeuona.
6.Naye kawabarikia, Yosefu naye Maria
Huku kimwonya Maria, machungu tayapitia.
"Upanga utaingia, ndani ya moyowo pia."
Wokovu lotuwekea, kwa macho tumeuona.
7.Alikuwa hekaluni, na nabii Ana pia.
Kwa miaka themanini, lisali kifunga pia.
Habari aliwapeni, Mungu kamshukuria.
Wokovu lotuwekea, kwa macho tumeuona.
8.Yote yalipotimia, kwa sheria yake Bwana.
Nazareti lirudia, waweze kulea mwana.
Neema ilimjia, na hekima huyu Bwana.
Wokovu lotuwekea, kwa macho tumeuona.
Na
Malenga Ibura
Bokeny Ochigo
28/12/2024.