Shairi Fundi wa kukuna nazi

แชร์
ฝัง
  • เผยแพร่เมื่อ 28 มิ.ย. 2018
  • **Fundi wa kukuna nazi**
    Jamani kila shetani, huwa na mbuyu wake
    Litieni akilini, wangwana msishituke
    Nami nabwaga makini, kisha chini niandike
    Ameimiliki mbuzi, fundi wa kukuna nazi.
    Mbuzi akishaishika, kifuvu hutetemeka
    Kwenye mbuzi huchomeka, kijasho kikimtoka
    Fundi amekamilika, kwao anaheshimika
    Ameimiliki mbuzi, fundi wa kukuna nazi.
    Nazi hukuniwa ndani, huku jungu latokota
    Hakunii hadharani, watu wakamwita ita
    Jasho kimwaga mwili, mkuna nazi hufuta
    Ameimiliki mbuzi, fundi wa kukuna nazi.
    Huikuna kwa ujuzi, huku akiimba imba
    Anaijulia kazi, namba wani anatamba
    Na hakuni kwa ufyozi, si mtu wa kujigamba
    Ameimiliki mbuzi, fundi wa kukuna nazi.
    Kifuvu hukitingisha, kikunwe kila upande
    Bila nazi kubakisha, na panza hata kipande
    Fundi huyu hunikosha, akunavyo chonde chonde
    Ameimiliki mbuzi, fundi wa kukuna nazi.
    Hakuni kwa kubambanya, ni jasiri kama chui
    Miguu huitawanya, mbuzi haimsumbui
    Akuna akiifinya, hadi inamwaga tui
    Ameimiliki mbuzi, fundi wa kukuna nazi.
    Nasita mwana wa mama, ama kungwi wa kiume
    Kama una la kusema, litapike uliseme
    Kukujibu sitogoma, najiamini kidume
    Ameimiliki mbuzi, fundi wa kukuna nazi.
    Ni yule yule
    Malenga Msema Kweli
    Abdulkarim Kuchengwa
    Mwana wa Mama
    Kungwi wa Kiume
    County 002, Coast Ke.
    ©2017
    #KungwiWaKiume #kuchengwa

ความคิดเห็น • 49